Uongozi wa Maafande wa Polisi Tanzania FC umesema umejipanga kuhakikisha kikosi cjao kinaonyesha kiwango bora katika mechi yake ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC itakayochezwa kesho Jumanne (Juni 06) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Polisi Tanzania FC inahitaji ushindi katika mechi hiyo huku ikiziombea timu nyingine zilizoko mkiani kupoteza michezo yao iliyobakia.
Akizungumza jijini Dar es salaam Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munisi, amesema wanafahamu Simba SC hawana cha kupoteza katika mechi hiyo lakini wao mchezo huo ni muhimu kwa sababu bado hawajakata tamaa.
Munisi amesema wamewaandaa wachezaji wao kupambana katika mechi hiyo kwa sababu uwezo wa kuondoka na alama tatu na kurejea katika ulingo wa mapambano.
“Sisi tupo I.C.U, lakini wenzetu Simba SC wao hawana cha kupoteza, tutahakikisha tunapambana ili kutoka I.C.U, ninaamini hilo linawezekama kufuatia tulivyokiandaa kikosi chetu,” amesema Munisi.
Ameongeza ushindani uliopo katika msimu huu umesaidia kuiboresha na kuipa thamani Ligi Kuu Tanzania Bara, ndio maana vita ya kuwania ubingwa ilikuwa ndefu huku hadi leo bado timu nyingine itakayoshuka daraja na zile zitakazocheza ‘play off’ hazijajulikana.
“Hatutashuka kinyonge, vijana wameahidi kujituma kama ambavyo wamefanya katika michezo iliyopita, tulifanya kila jitihada, tuliboresha kikosi chetu pamoja na benchi la ufundi tukiamini tujiondoa mkiani, haikuwa hivyo,” Munisi ameongeza.
Baada ya mechi hiyo, Polisi Tanzania itabakia Dar es Salaam kuwasubiri Azam FC katika mechi ya kumaliza msimu itakayochezwa Juni 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex.