Jeshi la Polisi Mkoani Arusha, limeungana na wadau ikiwemo Chuo cha ufundi Arusha pamoja Chama cha Mawakala wa waongoza Utalii nchini – TATO, kutoa mafunzo kwa madereva wa magari ya watalii katika kuelekea msimu wa utalii.

Mkuu wa usalama Barabarani mkoani humo Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Zauda Mohamed wakati akifungua mafunzo hayo amesema Jeshi hilo linatoa mafunzo hayo ili kuhakikisha usalama wa watalii ambao wataongezeka kwa wingi mkoani humo kuelekea msimu huo ambao unaanza hivi karibuni.

Amesema, mafunzo hayo yatawaongezea weledi madereva hao katika utendaji wao wa kazi ambao utafanikisha watalii wote wanaofika mkoani humo kuwa salama wakiwa barabarani na madereva hao wataelekezwa namna bora ya kuwasiliana na Polisi, ikiwa watapa changamoto za kiusalama pindi wanapokuwa barabarani na wageni.

Awali, Mkuu wa Kituo cha Polisi Utalii na Diplomasia Mrakibu wa Polisi, Waziri Tenga alibainisha kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais za kuutangaza Utalii ili kuongeza ujuzi na weledi kwa madereva hao katika kuhakikisha wanakua salama pindi wanapokuwa na watalii barabarani.

Naye, Daktari Yusuph Mhando ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia masuala ya Taalumu na Utafiti toka Chuo cha Ufundi Arusha amesema chuo hicho kipo tayari na kimejipanga katika kuhakikisha wanatoa mafunzo bora kwa madereva hao ili shughuli zao ziweze kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wake Sirili Akko, Katibu Mtendaji wa TATO amesema waliomba mafunzo hayo kufanyika ili kuwajengea uwezo madereva hao kabla ya kuanza kwa msimu wa utalii hivi karibuni ambapo wanatarajia kupokea idadi kubwa ya wageni huku Elias Laizer, dereva na muongoza watalii akisema mafunzo hayo yatawaongezea ujuzi na weledi ambao utapelekea kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

TPLB, TFF wamaliza utata Singida BS Vs Young Africans
Mayele: Mzamiru amenipigia na kuomba radhi