Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kukamata jumla ya pikipiki 825 na vifaa vingine, zilizokuwa zimeibwa katika mikoa nane nchini.
Pikipiki hizo zimekamatwa kufuatia amri iliyotolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro kufuatia kuongozeka kwa visa vya wizi wa pikipiki katika mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Mara (Tarime-Rorya) na Kagera.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana, Mei 30, 2020 na Kamanda wa Oparesheni Maalum za Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Mihayo Msikhela, oparesheni hiyo ilifanyika kuanzia Mei 4 hadi Mei 29, 2020, katika mikoa nane.
Alisema kuwa wakati wa oparesheni hiyo, walibaini kuwa wamiliki wengi wa pikipiki hawana mikataba ya maandishi na watu wanaoendesha pikipiki zao maarufu kama bodaboda. Pia, walibaini kuwa wapo ambao hawakuandikishana wakati wa kuuziana pikipiki; na wengine hawakubadili namba za usajili baada ya kununua kutoka kwenye makampuni husika.
Aidha, Kamanda Msikhela alisema kuwa walibaini kuwa baadhi ya wezi waliondoa namba za usajili halisi na kuweka namba za usajili batili kwenye ‘plate number’ za pikipiki zao.
Aliwataka wananchi kuhakikisha wanaripoti mara moja katika vituo vya polisi wanapohisi watu kuwa ni wezi au wana vitu ambavyo ni vya wizi.
“Ninawataka wananchi kuripoti polisi watu wanaowadhania kuwa ni wezi au majambazi kabla hawajatekeleza nia zao ovu, ili kuokoa mali walizotaka kuibiwa,” alisema Kamanda Msikhela.
Takriani kesi 354 zimefunguliwa katika Mahakama mbalimbali Kanda ya Ziwa zikihusisha wizi wa pikipiki na vifaa vingine.