Polisi nchini Algeria wameripotiwa kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamefunga njia ya kuingia kwenye ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Maelfu ya watu wanaandamana kupinga uamuzi wa Rais Abdelaziz Bouteflika mwenye umri wa miaka 81 kutangaza kugombea tena.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, maelfu ya watu wamesafiri umbali mrefu kujiunga na waandamanaji katika maeneo mbalimbali ya majiji hususan tangu Ijumaa.
Imeelezwa kuwa ni mamia kadhaa ya waandamanaji kati ya maelfu ndio waliokumbana na kizuizi cha polisi.
Jumapili iliyopita, mamia ya watu ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa vyuo na taasisi mbalimbali walitangaza kujiunga na maandamano hayo jijini Algiers.
Rais Bouteflika ambaye tangu mwaka 2013 alipatwa na tatizo la kiharusi, alikuwa anaonekana akiwa kwenye kiti cha matairi (wheelchair).