Polisi Mkoani Mwanza imelikamata gari aina ya Toyota Harrier ikiwa limebeba kilo 561 za mirungi baada ya kutelekezwa na dereva aliyekuwa akiliendesha kufuatia Polisi kulitilia shaka barabarani huku likimshikilia mmiliki wa gari hilo Malema Maswi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Ramadhani Ng’anzi amesema tukio hilo limetokea Juni 8, 2022 katika eneo la Itumbili lililopo Wilayani Magu muda mfupi baada ya dereva wa gari hilo ambaye jina lake halijatambulika kulitelekeza na kukimbia.
“Gari hilo lilikuwa inatokea Mara ilipofika kwenye kizuizi cha magari wilayani Magu askari walilitilia shaka wakalisimamisha lakini dereva alikaidi amri na kupita kizuzi jambo lililosababisha tairi kupasuka na dereva alisimamisha na kukimbia, upekuzi ulipofanyika tukakuta kuna mirungi,” amesema Ng’anzi.
Amesema jeshi hilo linamshikilia mmiliki wa gari hilo kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tuhuma za usafirishaji wa dawa hizo, wakati msako wa kumpata dereva aliyekimbia ukiendelea.
“Hiki ni kiwango kikubwa cha dawa za kulevya ambacho tunaamini kama kingeingia hapa jijini kingeleta madhara kwa wananchi Sheria ya dawa ya kulevya iko wazi kwamba chombo chochote kitakachotumika kwenye usafirishaji kinaweza kutaifishwa,” amesema Ng’anzi
Aidha, Kamanda Ng’anzi amesema kundi lililoathirika kwa kiasi kikubwa na matumizi ya dawa hizo mkoani humo ni vijana na kudai kuwa jeshi hilo linaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na madhara ya matumizi ya dawa hizo.
“Tumebaini kwamba wanawake nao wameanza kujiingiza kwenye matumizi ya dawa hizi, awali tuliamini ni watu waaminifu hii inaashiria kuna mmonyoko wa maadili kwenye suala hili tutasimamia sheria bila kuangalia jinsia ya mtu,” amesema Ng’anzi
Vitendo vya matumizi, usafirishaji na uuzaji wa madawa ya kulevya vimekuwa vikipigiwa kelele na Jeshi hilo sambamba na wadau mbalimbali nchini, kutokana na athari zinazowakumba watuamiaji na kupelekea kuharibu afya na kudhoofisha nguvu kazi ya Taifa.