Jeshi la Polisi Mkoani Arusha, limewakamata watuhumiwa 38 wanaojihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu, huku mmoja kati yao akikutwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kwa kutumia gari la kubebea mafuta.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine amesema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika operesheni iliyofanyika kuanzia Septemba 05 hadi Septemba 10, 2022.
Amesema, katika operesheni hiyo Setemba 10, 2022 katika mtaa na kata ya Kikwe wilayani Arumeru, walimkamata Allen Wilbard Kasamu (49), akisafirisha dawa za hizo za kulevya zenye uzito wa zaidi ya robo tani ambao ni kilo 390.75kg.
“Mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa anasafirisha dawa hizo za kulevya kwa kutumia gari aina ya Mitsubish Canter – Tanker ambalo ni maalumu kwa ajili ya kubeba mafuta ambapo alitumia mbinu za kupakia ndani ya tenki la mafuta ili asijulikane,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, Kamanda Masejo amesema katika tukio jinginePolisi walifanikiwa kukamata pikipiki 13 zilizokua zinatumika katika matukio ya uhalifu, gongo lita nane, bangi kilo 70 pamoja na kompyuta mpakato tatu.
Katika hatua nyingine, Kamanda Masejo amesema, Wananchi wa Mkoa huo wamejitokeza kusalimisha silaha na kutoa rai kwa wanaomiliki silaha kinyume cha Sheria kufika katika vituo vya Polisi ama ofisi za watendaji wa mitaa kuzisalimisha.