Jeshi la Polisi nchini limesema limejipanga kudhibiti shughuli za tohara kwa watoto wa kike, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka ambapo baadhi ya watu wameanza kuhamasisha vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto.
Hayo yamebainishwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jijini Dodoma.
Amesema, Jeshi hilo limebaini njia mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumika kuandaa tohara hizo ambapo katika Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya mzee mmoja amebainika kuandaa kadi za mialiko kuhamasisha shughuli za tohara kwa watoto wa kike jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu.
“Tunatoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa, wenyeviti wa vitongoji, mtaa, vijiji, watendaji wa mitaa, vijiji na kata na wananchi wema kuwa macho katika maeneo yao na kutokuruhusu vitendo hivyo vikiwepo vya ukeketaji kufanyika katika maeneo yao na pia watoe taarifa polisi wanapoona maandalizi au vitendo hivyo vikifanyika” Amesema Misime.
Katika hatua nyingine, Kamishna Misime ameonya vitendo vya watu kukiuka sheria za nchi ikiwemo utapeli kwa kigezo cha kutafuta fedha za kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka ambapo amesema Jeshi hilo litawashughulikiwa kwa mujibu wa sheria bila kujali nafasi zao katika jamii.
Aidha, Misime ameongeza kuwa Jeshi la Polisi limeanza kuchukua hatua kali zaidi za kuimarisha doria za barabarani ili kuwadhibiti watumiaji barabara ambao kwa makusudi wanavunja sheria za usalama barabarani na kupelekea ajali zinazoleta madhara kwa watanzania.