Ikiwa leo ni siku ya ugonjwa wa kiharusi duniani, imeelezwa kuwa vijana wapo kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kiharusi kwasababu wengi wanavuta sigara, wanakunywa pombe, wanakula chakula kupita kiasi na bila mpangilio, wanauzito mkubwa na wanatumia dawa zinazohatarisha maisha yao.

Hayo yameelezwa na daktari bingwa wa magonjwa ya ubongo, mishipa ya fahamu na uti wa mgongo upande wa upasuaji, Mugisha Clement kutoka Hospitali ya Aga khan na kubainisha kuwa umri wa watu kupata kiharusi umeshuka na sasa vijana wenye umri wa mika 30 na kuendelea wapo kwenye hatari hiyo.

“vyote vinasababishwa na mtu kupata shinikizo la damu, ukiwa na shinikizo la damu katika umri mdogo kuna uwezekano wa kupata kiharusi” amesema Dkt. Clement.

Amesema takwimu za shirika la afya duniani (WHO), zinaonesha kati ya watu wanne mmoja atapata kiharusi.

Ameeleza pia dawa namba moja ya kujikinga na kiharusi ni kufanya mazoezi na kushauri watu wajijengee tabia ya kufanya mazoezi angalau mara mbili au mara tatu kwa wiki.

Imeelezwa kuwa dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kushindwa kuongea na kuelewa, kupooza kwa ghafla au kupata ganzi usoni, mkono au mguu na mara nyingi hutokea upande mmoja wa mwili.

Siku ya ugonjwa wa kiharusi duniani huadhimishwa ili kusisitiza asili na uwepo wa ugonjwa huo, kuongeza uelewa wa kuzuia na kuhakikisha utunzaji bora na msaada kwa waathirika.

 

 

Ujio wa Mapadri waliooa utafanikiwa?
Afya ya Moi yatetereka tena