Klabu ya Azam FC imepania kufanya vyema msimu ujao 2023/24 ikiwemo kuanza kutwaa taji la Michuano ya Ngao ya Jamii, itakayorindima jijini Tanga.

Michezo ya Ngao ya Jamii inatarajiwa kuanza keshokutwa Jumatano (Agosti 09) katika Uwanja wa CCM Mkwakwani, ikishirikisha timu za Simba SC, Young Africans, Singida Fountain Gate na Azam FC.

Katika michuano hiyo itakayoanzia Nusu Fainali, Azam FC itachuana na Young Africans wakati Simba SC ikicheza na Singida Fountain Gate.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popati’, amesema kuwa timu yao ipo tayari kuanza msimu mpya na malengo yao ni kutwaa mataji mbalimbali ikiwemo Ngao ya Jamii.

“Timu yetu ipo vizuri na tumejipanga vya kutosha kwa msimu mpya, hatutarudia makosa kama ya msimu uliopita,” amesema Popati.

Amesema benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Youssouph Dabo, limeinoa vyema timu hiyo na anaamini watakuwa na msimu wa mafanikio.

Ikiwa Azam FC itaitoa Young Africans, itacheza na mshindi kati ya Simba SC na Singida Fountain Gate kuwania taji la Ngao ya Jamii mwaka huu.

Rais Samia kujenga viwanja Arusha, Dodoma
STAMICO yanyakua Tuzo Kampuni bora ya Madini 2023