Azam FC imeshtukia jambo na kuamua kumuongezea mkataba mshambuliaji wa timu hiyo Mzimbabwe, Prince Dube utakaomuweka kwenye viunga vya Chamazi hadi mwaka 2026.
Nyota huyo aliyemaliza msimu wa 2022/23 na mabao 12, tayari viongozi wa Azam wamempa dili hilo baada ya mkataba wake kubakia mwaka mmoja ambao ungemalizika 2024.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema mchezaji huyo amekuwa muhinu kwenye kikosi hicho hivyo wasingetamani kuona anaondoka kirahisi.
“Tuko kwenye wakati wa kuboresha timu kwa maana ya usajili mpya lakini wakati tukifanya hayo tunaendelea kuongezea mikataba mipya kwa wachezaji tunaoona watakuwa na msaada mkubwa kwa ajili ya msimu ujao,” alisema.
Dube alijiunga na Azam FC Agosti 2020 akitokea timu ya Highlanders ya nchini kwao na katika misimu mitatu aliyoichezea amefunga jumla ya mabao 27 kwenye Ligi Kuu Bara.
Mbali na Dube mastaa wengine walioongezewa mikataba mipya ni Idris Mbombo, Nathaniel Chilambo, Lusajo Mwaikenda, Abdallah Kheri ‘Sebo’, Malickou Ndoye, Daniel Amoah, James Akaminko na Sospeter Bajana aliyekuwa anawindwa na Simba SC.