Mshambuliaji wa Azam FC Prince Dube amesema mechi ijayo dhidi ya Young Africans itakuwa ngumu, lakini Azam FC haitaingia kinyonge kwa kuwa wanazitaka alama tatu.
Dube ndiye aliyefunga bao pekee lililoipa Azam ushindi wa mwisho mbele ya Young Africans katika Ligi Kuu kwenye mechi iliyopigwa Aprili 25, 2021, kabla ya mechi tano zilizofuata baadaye zikiwamo nne za ligi na moja ya Ngao ya Jami, Young Africans kushinda nne na mchezo mmoja kwisha kwa sare.
Dube amesema anajua matokeo ya mechi zilizopita zitawafanya kuonekana wanyonge mbele ya Young Africans, lakini mchezo wa Jumapili (Oktoba 22), Azam FC inataka kumaliza unyonge kwa kupata ushindi.
Amesema mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa kwani wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi wa kwanza ndani ya uwanja wa Azam Complex mbele ya wapinzani wao hao.
“Lazima tuendelee kuwa sehemu nzuri katika ligi kwani tuna timu bora yenye wachezaji wazuri. Hatukuanza ligi kwa kasi lakini kwa sasa timu imeendelea kuimarika tunataka kuendeleza kasi.
“Tunajua Young Africans ni timu nzuri na hivi karibuni tumekuwa hatupati matokeo mazuri mbele yao, lakini tunahitaji matokeo tofauti kwa timu yetu dhidi yao. Ili uwe bora unahitaji kushinda mechi kubwa kama hizi,” amesema.
Baada ya kupata majeraha kisha kucheza mchezo uliopita Dube sasa amerejea akiwa na afya nzuri.