Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi, amekutana na kupokea nakala za hati za utambulisho za mabalozi wateule nchini pamoja na hati ya utambulisho ya Konseli Mkuu wa China Zanzibar.
Mabalozi waliowasilisha nakala za hati za utambulisho kwa Prof. Kabudi katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ni Balozi mteule wa Namibia, Lebbius Tangeni Tobias na Balozi mteule wa Ireland, Mary O’Neil, pamoja na Konseli Mkuu wa China Zanzibar, Zhang Zhisheng.
Akiongea mara baada ya kupokea nakala ya hati ya utambulisho wa Balozi mteule wa Namibia, Prof. Kabudi amesema kuwa Tanzania na Namibia zimekubaliana kuendeleza kuimarisha sekta ya biashara na uwekezaji, mifugo na uvuvi katika bahari kuu pamoja madini kwa maslahi ya mataifa yote mawili.
“Tanzania na Namibia tuna historia inayofanana iliyoanza tangu vita vya ukombozi wa uhuru wa Namibia, wote tulikuwa makoloni ya Wajerumani, hivyo tumekubaliana kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji, na katika maeneo ya mazao ya mifugo, uvuvi, kilimo, na madini,” amesema Prof. Kabudi.
Kwa upande wake Balozi Mteule wa Namibia nchini, Lebbius Tangeni Tobias ameahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Namibia.
“Mimi kama mwakilishi wa Serikali ya Namibia nitajitahidi wakati wa utumishi wangu hapa Tanzania kuhakikisha kuwa uhusiano wetu sisi Namibia na Tanzania unazidi kuimarika kwa maslahi mapana ya wananchi wetu wote,” amesema Tobias.
Aidha, Prof. Kabudi amepokea nakala ya hati za utambulisho wa Balozi mteule wa Ireland nchini, Mary O’Neil ambapo mara baada ya kukabidhi hati za utambulisho, Balozi O’Neil ameahidi kuendeleza uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Ireland.
“Ni furaha kwangu kuwepo hapa leo na kukabidhi nakala ya hati ya utambulisho wangu hapa nchini Tanzania, napenda kuahidi kwa kipindi nitakachokuwa hapa nitahakikisha kuwa uhusiano wetu wa kidiplomasia unakuwa na kuimarika kwa maslahi ya mataifa yetu,” amesema Balozi O’Neil
Katika tukio jingine, Prof. Kabudi amekutana na kupokea hati ya utambulisho wa Konseli Mkuu wa China Zanzibar, Zhang Zhisheng ambapo amesema amesema kuwa China imekuwa ikiisaidia sana Zanzibar tangu mapinduzi ya mwaka 1964, katika maeneo mbalimbali kama vile ujenzi wa barabara, ujenzi wa shule, ukarabati wa uwanja wa ndege, hospitali ya Mnazi mmoja pamoja na miradi mingine.