Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara wanaotoa huduma katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) kulipa kodi ya Majengo kama mikataba yao inavyolekeza.
Ametoa agizo hilo mapema hii leo wakati alipokutana na wafanyabiashara hao ili kujadili changamoto mbalimbali zilizopo na jinsi ya kuzitatua ili kuendelea kutoa huduma bora katika uwanja huo.
“Kulipa kodi za majengo hapa ni suala la lazima, hivyo ifikapo Septemba mwishoni nataka kuona wafanyabiaashara wote mmeshalipa kodi ya pango, makusanyo haya ni muhimu kwetu ili tuendelee na hatua nyingine za uboreshaji wa viwanja vya ndege na huduma nyinginezo.” amesema Prof. Mbarawa
Mbarawa ameutaka uongozi wa Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania (TAA), Kuhakikisha mikataba yote ya upangishaji wa majengo inapitiwa upya na kufanyiwa marekebisho ili thamani ya fedha iendane na wakati huu.
Hata hivyo, amewahimiza wafanyabiashara hao kubadilika na kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ili kuweza kuendana na ushindani wa kibiashara uliopo ndani na nje ya nchi.