Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Rwekaza Mukandala amewataka vijana wanaohitimu kidato cha sita nchini wawe makini na wasikubali kusombwa na mawimbi ya dunia.
Prof. Mukandala amesema hayo wakati akizungumza na wahitimu 237 wa kidato cha sita wa shule ya sekondari ya St. Joseph Cathedral kwenye mahafali ya sita ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo, jijini Dar es Salaam.
“Kwa hatua mliyofikia kila mmoja anapaswa atafakari kwa kina wito wake kimaisha. Kuweni makini, msisukumwe na mawimbi ya dunia na kujikuta mmepoteza ndoto zenu,” amesema Prof. Mukandala.
“Kuhitimu kidato cha sita si jambo dogo. Ni hatua ya kuwaongiza kujiandaa na utu uzima ikiwemo kujiunga na elimu ya vyuo vya juu na kuingia kwenye ndoa. Ni muda wa kutathmini yale uliyopitia na kutafakari maisha yako ya baadaye. Ni fursa ya kutoa shukrani kwa Mungu, kwa wazazi na walimu ambao walifanya kazi kwa umakini na kujitoa ili mfikie hatua nzuri mliyopo sasa,” alisema.
Amesema kuanzia sasa kila mmoja wao anapaswa kujiamini, kujituma zaidi na kujiona kuwa ana wajibu wa kujiletea maendeleo binafsi. “Mnapaswa kuepuka mwenendo wa kujiona mnyonge, au mtu asiyeweza kutimiza ndoto zake. Jenga tabia ya kuwa makini na maisha yako, jali mazingira yako na maendeleo yako,” alisisitiza.
Prof. Mukandala amewataka wahakikishe wanakuchukua hatua mahsusi na kupata taarifa sahihi kuhusu taaluma wanazozitaka. Aliwataka wawe waadilifu na wenye heshima kwa watu wote lakini pia akawaasa juu ya maisha ya kutaka kupata fedha kwa haraka na kujilimbikizia mali.
“Epukeni rushwa na ufisadi. Mnatakiwa kujua kuwa utu, maendeleo na maisha bora havipatikani kwa fedha ingawa nayo ni muhimu katika maisha. Msitegemee kuishi kwa kuzingatia mambo makubwa yanayopimika kwa fedha,” alisema.
Wakati akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na hadhira iliyokuwepo, Mkuu wa Shule ya St. Joseph Cathedral, Sista Theodora Faustine alisema St. wanafunzi waliohitimu jana ni 237 ambao kati yao wavulana ni 140 na wasichana ni 97 waliokuwa wakichukua michepuo ya ECA, EGM, CBG, HGE, HGL, PCM, PCB na PGM.
Amesema anaamini kwamba wahitimu wote watakuwa na sifa za kujiunga na vyuo vikuu mwaka huu kwa sababu shule hiyo imekuwa ni ya kwanza yenye wingi wa ufaulu kuliko shule yoyote mkoani Dar es Salaam. “Tumekuwa tukipata wanafunzi bora kitaifa mara kwa mara na mwaka jana tulipata wanafunzi bora kutoka michepuo ya PCB na ECA,” alisema.
Sista Theodora amesema wamekuwa wakifaulisha wanafunzi zaidi ya 250 kwa mwaka na kwa maana hiyo, wameweza kuandaa vijana 250 kuingia kwenye vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi. Akifafanua kuhusu malengo ya shule, Mkuu huyo wa shule alisema lengo lao ni kutoa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania na kuwandaa kuwa wawajibikaji kwa Mungu na kwa Taifa lao.