Profesa Rita Jitendra wa India amefariki dunia akiwa anafanya mahojiano mubashara kwenye kituo cha runinga, akizungumzia maisha yake.
Profesa Jitendra ambaye ni mwandishi mashuhuri alikuwa kwenye kipindi cha ‘Good Morning J&K’, ambapo alikuwa akisisitiza kuwa angependa pumzi yake ya mwisho imtoke akiwa anafanya kazi zake. Lakini katikati ya sentensi hizo, alianguka ghafla.
Mtangazaji wa kipindi hicho, Zahid Mukhtar amesimulia, “wakati tunaendelea na mahojiano, akitueleza mambo mazuri kuhusu maisha yake na alikuwa anaonekana mwenye afya njema.”
“Lakini ghafla aliacha kuzungumza na baadaye kuanguka. Tulilazimika kusitisha mahojiano na kumkimbiza hospitalini lakini kwa bahati mbaya alipoteza maisha,” anakaririwa na Telegraph ya India.
Naye Hafiza Muzaffar aliyempeleka katika mahojiano hayo, alisema walipokuwa njiani alikuwa anasisitiza kuwa angependa kifo chake kiwe kama cha rais wa zamani, A.P.J Abdul Kalam.
Anasema alimwambia kuwa Dkt. Kalam alifariki dunia akiwa anafanya kazi na angependa iwe hivyo kwake pia.
Hospitali ya SMHS Hospital ya Jammu, India imeeleza kuwa kifo chake kimetokana na kubadilika ghafla kwa mapigo ya moyo katika hali isiyo ya kawaida, kwa jina la kitaalam ‘cardiac arrest’.