Rapa Eminem ameamua kuzungumzia mambo yaliyojili baada ya albam yake ya ‘Revival’ ya mwaka 2017 kuingia mtaani na kukutana na ukosoaji mkubwa.

Akifunguka katika mahojiano na Sway Collway, rapa huyo ambaye amesafisha njia kwa albam ya ghafla ya ‘Kamikaze’, iliyofanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwenye Billboard 200, amesema waliomkosoa wengi walivuka mstari.

“Sio kwamba sipokei ukosoaji ambao unajenga, lakini nahisi kama ukosoaji ulienda mbali zaidi ya ukosoaji wa kujenga,” alifunguka.

“Kama isingekuwa albam ya Revival, nisingeweza kutengeneza hii albam [Kamikaze]. Baadhi ya watu, na wengine zaidi walienda mbali kidogo na ukosoaji huo,” aliongeza.

Baadhi ya watu ambao walijikuta wameingia matatani na Eminem katika njia hiyo ya ukosoaji ni pamoja na Joe Budden na Machine Gun Kelly. Eminem aliwachana wote wawili kupitia ngoma yake ‘Fall’.

Marapa hao walimjibu pia kila mmoja kwa aina yake, Joe alijibu kupitia kipindi chake cha redio ya mtandaoni lakini Machine Gun Kelly yeye aliachia ‘diss track’ aliyoibatiza jina la ‘Rap Devil’.

Katika mahojiano hayo, Eminem alisema kuwa chanzo cha kuwavaa Budden na Kelly sio kumzungumzia binti yake Hailie kama wengi wanavyodhani.

“Hiyo haikuwa sababu ya kuwachana. Sababu ya kuwachana ilikuwa rahisi zaidi hata ya hiyo,” alifunguka.

Machine Gun Kelly alionekana kumuudhi Eminem mwaka 2012, alipoweka mtandaoni picha ya binti yake mwenye umri wa miaka 16 na kuandika maneno ya kumtamani.

Ni kama Kamikaze imemrejesha Eminem kileleni baada ya kuanguka kwenye Revival na huenda ndio sababu amekubali kufanya mahojiano kwani ni nadra kwake kufunguka kwenye vipindi vya redio/TV.

Profesa afariki ghafla akizungumzia maisha yake kwenye TV
TABOA, DataVision kuokoa mamilioni ya fedha nchini