Sakata la tuhuma dhidi ya Bernard Membe kuanza mapema mchakato wa kuwania nafasi ya kugombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi ujao, lililowekwa wazi na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Bashiru Ally limemuibua Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu.
Profesa Baregu ameeleza kuwa sakata hilo linatoa fursa chanya kwa kambi ya upinzani endapo halitatafutiwa ufumbuzi mapema, kwani inaonesha dhahiri kuwa ndani ya CCM bado kuna makundi.
“Membe [wa Twitter] amejibu vizuri kidiplomasia. Ila naona huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM ni kama kuna makundi sasa. Mambo yanaweza kuwa magumu kwa CCM kwa sababu wanaweza kupata mgombea ila asiungwe mkono na wanachama wake wakachukua hatua,” amesema Profesa Baregu.
Dkt. Bashiru amemuita Membe ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Serikali ya Awamu ya Nne na pia alikuwa miongoni mwa waliowania nafasi ya kugombea Urais kupitia CCM mwaka 2015.
Katibu Mkuu huyo wa CCM alimtaka Membe kufika ofisini kwake ili azungumze naye kuhusu tuhuma hizo, akiweka msimamo kuwa njia aliyotumia kumuita kupitia mkutano wake ni njia sahihi kwani hakuna mwanachama mwenye nguvu kuliko chama.
Mwanasiasa huyo amekuwa kimya tangu kumalizika kwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Hivi karibuni, alikuwa miongoni mwa makada wakongwe na viongozi wa CCM waliotuhumiwa na Syprian Musiba kuwa wanahujumu chama hicho, akitajwa kuwa anafanya vikao vya chinichini kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020.