Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Mahakama Profesa Elisante ole Gabriel, kuhakikisha haki za kweli kwa wananchi zinapatikana kwani muhimili huo kwa mujibu wa katiba ya Tanzania ndio mamlaka ya mwisho katika utoaji haki.
Ameyaagiza hayo leo Agosti 21, 2021 kwenye hotuba baada ya uapisho wa viongozi mbalimbali wateule akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama Profesa Elisante, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Aidha Rais Samia amemuagiza pia Profesa Elisante kuhakikisha Magereza hayajai watu wasio na makosa ikiwa na tafsiri ya kwamba haki itendeke, pamoja na hayo amempa jukumu la kusimamia watumishi wa Mahakama wafanye kazi katika mazingira mazuri na kuangalia maslahi yao.
Sambamba na hayo Rais Samia pia ametoa agizo la kuangalia namna gani wataweza kuzipeleka Mahakama zinazotembea katika maeneo mengine kwa wingi zaidi kutokana na Mahakama hizo kuwa na mrejesho mzuri wa huduma hasa katika upande wa vijini.
Hata hivyo Rais Samia amewakumbusha viongozi hao kuwa majukumu waliyonayo mbele ya watanzania ni makubwa hivyo hawana budi kufanya kazi kwa bidii.