Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amemshutumu tena Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif akidai kuwa alidekezwa na kuvaa kiburi.
Profesa Lipumba ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua kikao cha Baraza Kuu katika ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa kudekezwa huko ndiko kumesababisha afanye maamuzi ambayo yamekigharimu chama hicho kwa kushindwa kuwa na wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi visiwani Zanzibar.
“Tumemdekeza kwa muda mrefu. Na zile nyimbo tulizokuwa tunaimba kwamba ‘akipata Seif tumepata wote’, yeye alizitafsiri kuwa ‘akikosa Seif tumekosa sote’. Matokeo yake tumekosa kuwa na uwakilishi katika Baraza la Uwakilishi,” alisema Profesa Lipumba.
Aliongeza kuwa chama hicho kimewakosea Wazanzibar na kwamba uamuzi wa Maalim Seif umeharibu hali ya kisiasa Zanzibar.
Tamko la Profesa Lipumba limepingwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui ambaye anamuunga mkono Maalim Seif.
Mazrui amesema kuwa Maalim Seif hakudekezwa bali anaringia kura za Wazanzibar alizozipata katika uchaguzi mkuu uliopita.