Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar – SMZ, Dkt. Saada Salum Mkuya amekiomba Chama cha Waajiri Tanzania – ATE kuangalia uwezekano wa kupeleka hadi ngazi ya chini zaidi Programu ya Mwanamke Kiongozi, ili iweze kuibua vipaji vingi zaidi.
Dkt. Saada ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wawakilishi Wanawake Zanzibar – UWAWAZA ameyasema haho wakati wa Mkutano Mkuu wa Tano wa Mwanamke Kiongozi kwa mwaka 2023 uliofanyika kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Amesema, “Chama hiki cha Waajiri Tanzania, kiangalie uwezekano wa kushuka hadi shule za sekondari na vyuo vikuu ili kuibua vipaji vya wanawake wengi zaidi.”
Awali, Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Doran alisema tangu waanze programu hiyo kwa kushirikiana na ESAMI, tayari wametoa mafunzo kwa wanawake 274 kutoka kampuni 79 wakiwemo Wabunge na wawakilishi 150.