Klabu bingwa nchini Ufaransa PSG imetuma taarifa yenye kurasa tano ya malalamiko kuhusu mchezo wa hatua ya 16 bora wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya FC Barcelona, uliopigwa juma lililopita kwenye uwanja wa Camp Nou.

PSG wamelalamikia maamuzi mabovu ambayo wanadai yalichangia ushindi wa mabao sita kwa moja, ulioivusha FC Barcelona na kutinga kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Mwamuzi Deniz Aytekin ametajwa katika malalamiko hayo ya PSG, kama kichwa cha matatizo yote ambayo yalionekana kwenye mchezo huo ambao kwa asilimia kubwa uliwashangaza wadau wa soka ulimwenguni, kutokana na hitaji la FC Barcelona la kusaka ushindi wa zaidi ya mabao manne kukamilika.

Uongozi wa PSG umeeleza kusikitishwa maamuzi ya mwamuzi huyo kutoka nchini Uturuki, na unahisi kulikua na sababu za nyuma ya pazia, ambazo zilimsukuma kutoa maamuzi ya utata wanayodai yaliisaidia FC Barcelona kupata ushindi wa mabao sita kwa moja.

Sehemu ya malalamiko ya PSG ambayo yameorodheshwa kwenye taarifa yenye kurasa tano iliyowasilishwa huko UEFA, inadai katika mchezo huo kiungo kutoka nchini Argentina Javier Mascherano aliunawa mpira dakika 10 kabla ya mchezo kumalizika, baada ya kupigwa na kiungo Julian Draxler kuelekea katika eneo la hatari la FC Barcelona, na mwamuzi Deniz Aytekin alishindwa kupuliza kipyenga kwa kuashiria kosa hilo limefanyika.

Kadi ya pili ya GERARD PIQUE – PSG wamedai kuwa, beki huyo kutoka nchini Hispania alipaswa kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kisha nyekundu katika dakika ya 41, kufuatia kitendo cha kumvuta jezi kwa makusudi mshambuliaji wao Edinson Cavani, lakini haikuwa hivyo.

Penati iliyokwamishwa wavuni na Neymar – Hapa mwamuzi Aytekin kuizawadia penati ya upandeleo FC Barcelona kwa madai ya beki wa upande wa kulia wa PSG Thomas Meunier alimfanyia madhambi mshambuliaji huyo kutoka Brazil, jambo ambalo linapingwa na mabingwa hao wa Ufaransa.

Kujiangusha kwa Luis Suarez – Luis Suarez anadaiwa kujiangusha katika eneo la hatari kwa kisingiozio cha kufanyiwa madhambi na Marco Verratti. Lakini PSG wamesisitiza tukio hilo halikua na uhalali wa kusababisha adhabu.

Pique Kuushika Mpira – PSG wamedai kuwa mshambuliaji wao Angel di Maria alishindwa kufikia lengo la kupiga mpira uliokua unaelekea langoni mwa FC Barcelona, baada ya Pique kuushika mpira kwa makusudi katika eneo la hatari, na mwamuzi hakuchukua maamuzi yoyote.

Penati Ya Suarez – PSG wamelalamika kwa kueleza mkwaju wa penati uliopigwa na Neymar baada ya Luis Suarez kuonekana aliangushwa kwenye eneo la hatari, haikuwa sahihi kufuatia beki wa mabingwa hao wa Ufaransa Marquinhos kuanguaka sambamba na mshambuliaji huyo wa Uruguay.

Yusuf Manji Kupanda Tena Kizimbani
Floyd Mayweather Kurudi Ulingoni Juni 10