Mabingwa wa soka Ufaransa Paris Saint-Germain, wametangaza vita ya kuiwania saini ya beki wa FC Bayern Munich, David Alaba ikimtazama kama mbadala sahihi wa beki wao Thiago Silva, atakayeondoka klabuni hapo mara baada ya msimu huu kwisha.
Mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Leonardo amethibitisha kuwa wataachana na Silva katika msimu wa usajili wa majira ya kiangazi na wanamtazama David Alaba kama mbadala wake sahihi.
Mkataba wa Alaba kwa sasa umebakiza miezi 12 na baada ya miezi sita atakuwa huru kusaini makubaliano ya awali na timu nyingine kwani kanuni za usajili zinarhusu.
Lakini ripoti zinadai kwamba PSG, hawahitaji kusubiri hadi muda huo ufike ili wampate beki huyo mwenye umri wa miaka 27, hivyo wanafanya jitihada zote kuhakikisha wanaipata saini yake katika usajili wa nyakati za kiangazi mra baada ya ligi msimu huu kumalizika.
Alaba ni moja ya wachezaji ambao wana uwezo mkubwa wa kushambulia na kuzuia kwa wakati mmoja tofauti na mabeki waliopo PSG kwasasa ambao wamekuwa na ufanisi kwenye eneo moja tu.
Ingawa Bayern wenyewe wameweka wazi kuwa hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo, lakini hawatakuwa na nguvu ya kumbakisha ikiwa atalazimisha kuondoka kwenye mwaka wake wa mwisho wa mkataba wake.
Mkurugenzi wa michezo wa Bayern Hasan Salihamidzic, mapema wiki iliyopita alinukuliwa akileza namna wanavyotamani kumuona beki huyo akibaki ndani ya kikosi chao siku za usoni.
“Tayari kuna mazungumzo mafupi yameshafanyika, na tutaendelea pia kuongea nae, lakini kwa sasa tumejikita zaidi kwenye ‘Bundesliga’.
Kila jambo lina wakati wake. Tutajaribu kutumia kila kitu ili kuhakikisha anabaki na sisi kwa muda mrefu zaidi. David anajua nini anahitaji kutoka kwetu na sisi pia hivo hivo,” amesema mkurugenzi huyo wa michezo wa Bayern.