Kiungo Mshambuliaji (Winga) kutoka nchini Algeria na Klabu ya Manchester City, Riyad Mahrez anaendelea kusalia kuwa mchezaji anayewindwa na klabu ya Al Ahli inayoshiriki Ligi Kuu Saudi Arabia.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 alipoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza kuelekea mwisho wa msimu wa 2022/23 na hakufurahishwa na kukaa benchi wakati City wakishinda taji la FA na fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Imefahamika kuwa Mahrez alikuwa akiwasiliana na Al Ahli mwishoni mwa mwezi Juni, klabu hiyo ikiwa tayari kumlipa Pauni Milioni 45 kwa mwaka. Yeye yuko wazi kwa hatua kama hiyo.
Kama ilivyokuwa mwezi uliopita, City bado wanasitasita kumwacha Mahrez aondoke, huku mustakabali wa Bernardo Silva ukizidi kutokuwa na uhakika na ndio sababu kuu ya kutofanya uamuzi.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno ameomba akubaliwe uhamisho wa majira ya joto na PSG wanataka kumfanya kuwa mmoja wa wachezaji wa kwanza kusajiliwa na kocha, Luis Enrique.
Mchezaji mwingine ambaye yuko kwenye rada za Saudi Arabia ni beki wa kati wa City, Aymeric Laporte.
Hapo awali iliripoti Laporte alikuwa akiwindwa na Aston Villa na Tottenham Hotspur, lakini City haijapokea ofa yoyote kubwa kutoka kwa klabu hizo.
Huku nia kutoka Ulaya haijajitokeza, City iko tayari kumuuza kwa wanunuzi walio tayari kutoka Saudi Arabia, huku Al Ahli wakiwa tayari kumpa njia ya kuondoka.
Al Ahli pia wanamtaka kiungo wa SSC Napoli, Piotr Zielinski, ambaye anasakwa na SS Lazio kuchukua nafasi ya Sergej Milinkovic-Savic aliyejiunga na Al Hilal.