Pamoja na kuwindwa na klabu mbalimbali Barani Ulaya, mshambuliaji kutoka nchini Ureno Rafael Leao, amesema anatamani kuendelea kusalia katika klabu ya AC Milan ya Italia.
Nyota huyo ambaye juzi aliiongoza timu yake kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Napoli katika mchezo wa marudiano, anawindwa na klabu za Chelsea na Real Madrid.
AC Milan imetinga nusu fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1, baada ya mechi ya kwanza kushinda bao 1-0 katika Uwanja wa San Siro jijini Milan.
Leao, ambaye alizawadiwa tuzo ya mchezaji bora katika mchezo wa juzi, alipoulizwa kuhusu hatma yake katika klabu hiyo, alisema bado anafuraha na anahitaji kuendelea kusalia.
Alisema bado anaendelea na mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo kuhusu kuongeza mkataba, ambapo mkataba wake wa sasa unamalizika mwakani.
“Nataka kubaki hapa Milan, ndiyo. Lakini kuna mambo ya kuyaweka sawa,” Leao aliiambia Sky Sport Italia.
“Bado nipo chini ya mkataba kwa mwaka mmoja zaidi, tupo katika mazungumzo. Nahisi nipo nyumbani hapa AC Milan. Nina furaha kuwa hapa,” alisema.
Nyota huyo alisema bado anahitaji kuendelea kuisaidia timu hiyo kufanya vyema zaidi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.