Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) kwa sasa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Ismail Aden Rage, amesema mchakato wote wa uchaguzi wa Shirikisho hilo, umefanyika kwa kufuata taratibu zote za sheria na kanuni, tofauti na baadhi ya watu wanavyolalamika.

Rage ametoa maoni yake kuhusu Uchaguzi Mkuu wa TFF, huku Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam ikithibitisha kupokea kesi ya kupinga uchaguzi huo.

Taarifa iliyotolewa jana jioni imedai kuwa Mahakama hiyo ilimtaka Rais wa TFF Wallace Karia, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi na Bodi ya Wadhamini ya Shirikisho hilo kufika Mahakamani hapo maoema hii leo kujibu hoja za kwa nini uchaguzi wa TFF usisimamishwe.

Rage amesema amesoma sheria na kanuni zote za Uchaguzi wa TFF na kubaini hakuna tatizo lolote ambalo linaweza kukwamisha mchakato ambao unaendelea chini ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

“Mimi nimesoma sheria na kanuni zote za uchaguzi, kamati iko sahihi kabisa. Hawajakosea, na nimeona hata wagombea wenyewe wamekiri na kukubali,” alisema Rage.

“Kuongoza soka ni kazi ngumu. Sisi tumepita pale, tunajua hilo. Huwezi kutoka tu huko na kuwa kiongozi wa soka, kwa hiyo nawashauri wawe wanajipanga kweli,” amesema

Ameongeza kuwa kati ya wagombea wote ambao walijitokeza safari hii, mtu ambaye alikuwa ana uwezo wa kumtikisa Karia ni mwanasoka wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay.

“Yule alikuwa na uwezo wa kuongoza, lakini kwa bahati mbaya alishindwa mwanzoni. Na Kamati ilikuwa sawa tu tangu mwanzoni, kwani ilikuwa ikifanya hivyo kutokana na kanuni zilizopitishwa na wajumbe wenyewe,” amesema Rage.

Uchaguzi Mkuu wa TFF umepangwa kufanyika Agosti 07 jijini Tanga, kama Mahakama haitositisha mchakato huo.

Nabi achimba mkwara Dar Derby
Kesi ya sabaya yafika hapa leo