Aliyekua Mwenyekiti wa klabu ya Simba SC Ismail Aden Rage ameingilia kati sakata la madai ya mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Young Africans Amis Tambwe kwa kusema viongozi wengi wa soka nchini wamekua wakipuuzia kusoma kanuni, sheria za FIFA na CAF pamoja na mabadiliko yake, kiasi cha kushindwa kujua namna ya kuingia mikataba na wachezaji.
Tambwe aliifikisha Young Africans FIFA kwa kushataki juu ya deni lake la zaidi ya shilingi milioni 40, ambalo lilipaswa kulipwa kabla ya kuaachana na klabu hiyo misimu mitatu iliyopita.
Rage amesema viongozi wengi wa soka la Bongo wanafanya makosa wanapoingia madarakani, wanadhani madeni ya nyuma hayawahusu, kwa kudhani madeni ya nyuma hayawahusu ili hali wamekubali kuwa viongozi wa taasisi inayodaiwa.
“Watanzania wengi hatupendi kusoma, hatusomi kanuni, sheria za FIFA, na CAF, hatufuatilii mabadiliko mapya kupitia FIFA News, CAF News , kazi yetu ni kushindana shindana tu, na tunadhani kubishana kijeuri jeuri ndiyo itatusaidia katika kuendeleza mpira.”
“Kwa suala hili la Tambwe, inasikitisha na hili ni kosa la viongozi wetu wa vilabu kudharau mikataba. Nawashauri Young Africans wasifanye masihara, nasikia hata kuna mchezaji mwingine wa Zambia huko na kocha wanadai, ni bora walipe ili yaishe”
“Wakishalipa hiyo pesa adhabu itafutwa, kwenye mpira kuna kitu kinaitwa ‘fair play’ na FIFA hawataki kuumiza watu, hivyo pesa ikilipwa hawatofungia. Shida yetu sisi hatusomi, ukiwauliza viongozi wengi hivi sasa sijui kama wanajua sheria za mikataba za FIFA.” Amesema Rage.