Wananchi wa Malawi, leo Juni 23, 2020 wanashiriki uchaguzi mkuu wa marudio uliolenga kumchagua Rais, baada ya Mahakama kufuta matokeo ya uchaguzi wa awali uliompa ushindi Rais Peter Mutharika.
Mahakama ya Katiba ya Malawi ilieleza kuwa uchaguzi huo uliofanyika Mei 2019 haukuwa huru na haki na kwamba kanuni nyingi za uchaguzi zilikiukwa. Mahakama hiyo iliamuru uchaguzi wa marudio kufanyika ndani ya kipindi cha siku 150 kuanzia Februari 2020 hukumu hiyo ilipotolewa.
Milango ya vituo vya kupigia kura ilifunguliwa leo saa 12 asubuhi na inatarajiwa kufungwa saa 10 jioni. Watu milioni 6.6 wamejiandikisha kupiga kura.
Uamuzi huo wa Mahakama ya Katiba uliifanya Malawi kuwa nchi ya pili barani Afrika kufutiwa uchaguzi na mahakama. Kenya ilikuwa nchi ya kwanza baada ya Mahakama kufuta matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2017 na kulazimika kurudia.
Leo, uchaguzi utawakutanisha tena Rais Mutharika na mpinzani wake mkuu, Lazarus Chakwera ambaye kwenye uchaguzi wa Mei 2019 alizidiwa kura 159,000.
Tume ya Uchaguzi ilimtangaza Mutharika kuwa mshindi kwa asilimia 38.5 ya kura zote dhidi ya Chakwera aliyepata asilimia 35.