Rais wa Kenya, William Ruto amemtupia kijembe Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga akidai anatumia maandamano kutafuta suluhu na kwamba mbinu anayoitumia ni dalili za kutaka serikali ya nusu mkate na yeye kamwe hatakubali.
Akizungumza na wakazi wa Mutindwa katika Kaunti ya Tharaka Nithi, Ruto hata hivyo alisisitiza kuwa hatakubali suluhu hiyo akisema upinzani ni lazima ujifunze kukubali matokeo ya kura ya urais na kile kilichoamuliwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.
“Alisumbua sana Serikali ya Marais wastaafu Daniel Arap Moi na Mzee Mwai Kibaki (ambao kwa sasa ni marehemu), na pia Uhuru Kenyatta, kwa kutaka handisheki. Sasa tena anataka handisheki. Mimi sitakubali,” aliwaambia wakazi hao wa Mutindwa Rais Ruto.
Katika ziara hiyo, Rais Ruto alikuwa ameandamana na naibu wake Rigathi Gachagua ambapo kauli yake ni wazi sasa inafuta uwezekano wa salamu za maridhiano kati yake na Odinga, huku akimlaumu kiongozi huyo wa upinzani kwa kile alichodai ni kuwatumia vijana vibaya kutekeleza uharibifu wa mali na biashara.