Mgombea urais wa Kenya anayeungwa mkono na umoja wa vyama vya upinzani wa NASA, Raila Odinga ameituhumu Tume ya Uchaguzi nchini humo kwa kuandaa mbinu chafu dhidi yake ya kuchapisha karatasi za ziada za kupigia kura.
Mwanasiasa huyo mkongwe amedai kuwa mbinu hiyo pia ilitumika wakati wa uchaguzi wa mwaka 2013, na kwamba ndio sababu kuu ya Tume hiyo kusisitiza Kampuni ya Al Ghurair kuchapisha karatasi, kitendo ambacho kambi hiyo ya upinzani imekipinga mahakamani.
Akizungumza jana wakati akiupokea ugeni wa viongozi kutoka Kiambu jijini Nairobi kwa lengo la kuanza ziara ya kuwatembelea wapiga kura leo, Odinga alikejeli wito uliotolewa na Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake, William Ruto kumtaka mgombea wake mwenza Kalonzo Musyoka kumtelekeza na kujiunga na kambi la Jubilee.
Odinga alisisitiza kuwa NASA imepanga kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kijamii nchini Kenya na kwamba Jubilee hawatashinda uchaguzi wa Agosti 8.
“NASA ni sura ya Kenya. Nchi hii inakwenda kushuhudia mapinduzi ya kijamii na kiuchumi. Tuko kwenye hatua za kufanya mageuzi ya nchi. Tunataka kuwaeleza wapinzani wetu kwamba mabadiliko yanakuja. Jubilee hawawezi kushinda. Tunaenda kuzungumzia mambo yanayowaletea madhara Wakenya. Tutawaambia tuna suluhisho,” alisema Odinga.
Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya alieleza kuwa NASA wataanzisha safari Julai 7 mwaka huu, Uhuru Park itakayoongozwa na maombi na kisha kuelekea kwenye uwanja wa Kamukunji kwa ajili ya sikukuu ya Sabasaba.