Baada ya shambulizi la risasi na mabomu lililoua Watu 21 na kujeruhi 117 Hotelini nchini Somalia, Rais Hassan Sheikh Mohamud ameahidi vita kali ya kutokomeza Kundi la Al-Shabaab.
Katika taarifa yake ya kwanza kwa taifa tangu wanamgambo hao wa kiislamu kufanya uvamizi mkubwa wa saa 30 kwenye hoteli moja mjini Mogadishu Sheikh Mohamud amesema nia ya serikali ni kutokomeza maombolezo yasiyoisha kutokana na ugaidi wa Alshaabab.
Amesema “Ninajua kwamba wananchi wa Somalia wamechoshwa na rambirambi na maombolezo yasiyoisha, najua kwamba mnawapoteza watu wenye thamani katika kila shambulio linalofanywa na magaidi,” Mohamud amesema.
“Tuna dhamira ya kuwadhoofisha magaidi wanaoteketeza wanainchi wetu hadi maeneo yote wanayoyadhibiti yamekombolewa, hili ni jambo la kipaumbele kwa serikali yetu na maandalizi na utelekelezaji wa mpango huo unaendelea,” ameongeza.
Shambulio hilo ambalo lilianza Ijumaa jioni, lilikuwa ndilo kubwa zaidi kuukumba mji mkuu wa Somalia tangu Mohamud aingie madarakani Juni 2022 na kusisitiza changamoto ya kujaribu kumaliza uasi wa miaka 15 wa kundi lenye uhusiano na Al-Qeada.
Watu 21 walifariki na wengine 117 kujeruhiwa katika shambulio hilo la bunduki na mabomu lililolenga hoteli maarufu ya Hayat, na raia wa Norway ni miongoni mwa waliokufa, kwa mujibu wa serikali ya Norway.