Waziri wa Afya wa Somalia Dkt. Ali Haji Adam amesema idadi ya vifo vilivyotokea katika Hoteli ya Hayat mjini Mogadishu, imefikia watu 21 huku wengine 117 wakijeruhiwa kati ya Ijumaa jioni na Jumamosi usiku.

Waziri Adam ameyasema hayo wakati akihojiwa na vyombo vya Habari na kuongeza kuwa raia kadhaa, waliokuwa wamekwama katika hoteli hiyo waliokolewa wakati na baada ya kuzingirwa kwa saa 30 na vikosi vya usalama, vitengo vya dharura na maafisa wa Polisi waliokuwa wakiilinda hoteli hiyo.

Amesema, “Wakati wa operesheni hizo, vyombo vya usalama vililenga kuwaondoa raia waliokuwa ndani ya Hoteli na walifanikiwa kuokoa zaidi ya watu 106 wakiwemo watoto na wanawake.”

Kwa upande wake, Kamishna wa Polisi wa Somalia, Meja Jenerali Abdi Hassan Mohamed alisema Hoteli hiyo ilipata uharibifu mkubwa wakati wa mapigano ya risasi kati ya wanajeshi wa Somalia na magaidi hao.

Amesema, Polisi pia walilazimika kukagua jengo hilo kwani walihofia baadhi ya vilipuzi vinaweza kufichwa ndani ambapo siku ya Jumapili (Agosti 21, 2022) Wananchi wengi walikuwa wakisubiri kujua hatma ya jamaa zao waliopotea.

“Kilichotokea hapa ni maafa, kinatuathiri katika ngazi mbili kwani baadhi yetu tunawafahamu watu waliofariki na wanakabiliwa na uharibifu wa mali, kuzingirwa kwa hoteli hiyo kulidumu kwa takriban saa 32, vikosi vya usalama na al Shabaab vilipigana juu yetu,” amesema Meja Jenerali Mohamed.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Abdiqani Ali Adam mkazi wa Mogadishu alieleza kuwa, “Kama unavyoona kuna mali nyingi zilizobomolewa hapa, matukio kama haya yanajirudia mara kwa mara na sisi kama vijana, ndiyo wahanga wa mashambulizi kama haya.”

Hoteli ya Hayat ni mahali ambapo Maafisa wa Serikali wanapendelea kukutana kwa ajili ya mambo mbalimbali, na Wanamgambo wa Al-Shabaab wamekuwa wakiwavizia ili kuwashambulia kwa zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Shambulio hilo linatajwa kuwa ni baya zaidi kuwahi kutokea na kufanywa na kundi lenye uhusiano na al-Qaeda tangu rais mpya wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud aingie madarakani mapema wezi Mei, 2022.

Dejan: Ninaamini mambo mazuri yanakuja Simba SC
Victor Akpan: Nilijua Simba SC kuna Presha