Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari amemsimamisha kazi Jaji Mkuu, Walter Samuel Nkanu Onnoghen ikiwa ni wiki tatu kabla nchi hiyo kufanya uchaguzi mkuu.
Ikulu ya Nigeria imeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kufuatia madai kuwa Jaji Mkuu alishindwa kutangaza mali na madeni binafsi kabla ya kuanza kufanya kazi hiyo mwaka 2017.
Rais Buhari amemchagua Tanko Mohammed kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa nchi hiyo katika kipindi ambacho Jaji Mkuu anaendelea kuchunguzwa.
Hata hivyo, Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani wameikosoa wakidai kuwa ina dalili za kutaka kuchanganya mchakato wa uchaguzi mkuu unaoelekea ukingoni.
Jaji Onnoghen amesimamishwa ikiwa ni saa 24 tu kabla ya kuwaapisha wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“Uamuzi wa kumsimamisha Jaji Mkuu umesababisha wananchi wengi wa Nigeria, ikiwa ni pamoja na wanasheria na waangalizi wa masuala ya kijamii kuhoji endapo hatua stahiki zilizingatiwa,” imeeleza taarifa ya Umoja wa Ulaya ambayo Dar24 imeiona.
Mpinzani wa Rais Buhari katika uchaguzi huo utakaofanyika mwezi ujao, Atiku Abubakar ameuita uamuzi huo kuwa wa kidikteta
Baadhi ya viongozi wa upinzani wameanza kampeni maalum ya kupinga hatua hiyo ya kusimamishwa kwa Jaji Mkuu, katika kipindi ambacho Rais Buhari amekuwa akidai kuwa Mahakama inamrudisha nyuma katika vita yake dhidi ya rushwa.
Marekani imeeleza kuwa inashangazwa na hatua hiyo kwani haikushirikisha mfumo wa kimahakama katika kufikia uamuzi.
Rais Buhari anakabiliwa na upinzani mkali kutoka katika uchaguzi ujao, anapojaribu kuwashawishi wananchi wa Nigeria kumchagua tena kuongoza nchi hiyo kwa mhula wa pili.