Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameridhia kuendelea kutolewa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.
Majaliwa ameyasema hayo Agosti 05, 2022 wakati akizungumza na wananchi baada ya kutembelea mradi wa ujenzi kituo cha afya cha Iglansoni akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo Wilayani Ikungi Mkoani Singida.
Amesema, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha huduma za jamii zinazotolewa nchini zinakuwa endelevu, na hivyo amewataka wananchi waendelee kuiamini na kuipa ushirikiano.
Akiongea wakati wa ziara hiyo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (OR-TAMISEMI), David Silinde amesema kituo cha afya cha Iglansoni ni miongoni mwa vituo vya afya 234 vinavyojengwa nchini kwa lengo la kusogeza karibu huduma za afya kwa wananchi.
Amesema, “Serikali imetoa shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa hospitali ya kisasa katika wilaya hiyo lakini mbali na Serikali kutoa fedha hizo pia, Mheshimiwa Rais Samia ameridhia shilingi bilioni 13.348 zitumike kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 667, Ikungi.”
Naye, Mkuu wa mkoa wa Singida, Peter Serukamba amesema anataka mkoa huo uwe wa kwanza kwa wananchi wote kuwa na bima ya afya, ili wawe na uhakika wa kupata huduma na kuwahamasisha kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa pia ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi juu ya kushiriki kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, linalotarajia kufanyika nchini kote Agosti 23, 2022.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Murro amemshukuru Rais Samia kwa kuridhia kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani humo zikiwemo shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa vituo vinne vya afya ili kusogeza huduma kwa wananchi.
Mkuu huyo wa wilaya amesema, ” Tunaahidi kuendelea kushirikiana na viongozi ndani ya wilaya kuhakikisha fedha zote za maendeleo zinazotolewa na Serikali zinatumika katika utekelezaji wa miradi husika kama iliyokusudiwa.”
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi amesema ujenzi wa kituo hicho cha afya cha Iglansoni kinachotarajia kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwezi huu umefikia asilimia 98 na umegharimu shilingi milioni 500.
Amesema kituo hicho kinatarajia kuwahudumia wakazi 13,608 wa vijiji vya Iglansoni na Mnyange ambapo mradi huo unahusisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, maabara, kichomea taka, jengo la upasuaji, wodi ya mama na mtoto na jengo la kufulia.