Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera ametangaza wiki mbili za maombolezo ya kitaifa baada ya watu zaidi ya 200 kuuawa na Kimbunga Freddy, ambacho kilipeleka maafa makubwa zaidi katika jiji la Blantyre na maeneo mengine ya kusini mwa nchi hiyo.
Kupitia hotuba yake ya kitaifa, Rais Chakwera amesema, “kutokana na ukubwa wa vifo vilivyosababishwa na maafa haya, nimeamua sisi sote kama taifa kufanya siku 14 za maombolezo na bendera zote zipeperushwe nusu mlingoti kwa siku saba za mwanzo.”
Awali iliripotiwa vifo vya watu 99 idadi ambayo iliongezeka na kufikia watu 190, ambapo katika kitongoji cha Chilobwe kilichopo karibu na Blantyre, wakazi wengi walisimama mbele ya mabaki ya nyumba zilizosombwa na maporomoko ya udongo huku upepo ukipungua, lakini mvua haikukoma.
Takriban watu 20,000 nchini humo wameathiriwa na hali mbaya ya hewa, na Ofisi ya Taifa inayohusika na Kukabiliana na Majanga nchini Malawi imetangaza katika taarifa inaarifiwa kuwa, watu 584 wamejeruhiwa na 37 hawajulikani waliko.