Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga, kufuatia vifo vya watu 19 vilivyotokea kwa ajali ya gari Wilayani Mufindi.
Ajali hiyo ya alfajiri ya leo Juni 10, 2022, imehusisha basi dogo la abiria lililokuwa likitokea Dar es salaam kuelekea Iringa baada ya kugonga lori lililokuwa limeharibika barabarani katika eneo hilo.
Akizungumzia kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi amesema watu hao 19 waliofariki Wanaume ni 14, Wanawake wanne na Mtoto mmoja wa wakike.
“Ajali ni kweli imetokea na kuna taarifa za majeruhi na vifo na kati ya waliofariki yupo mtoto mmoja wa kike na watu wazima 18,” alisema Kamanda Bukumbi.
Amesema wakati majeruhi wakiendelea kuokolewa ndipo lilikuja Lori jingine lililopoteza mwelekeo na kuligonga tena basi dogo na majeruhi, na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.
Awali, Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mafinga, Dkt. Victor Msafiri alithibitisha kupokea miili ya marehemu hao na majeruhi nane, na kusema wawili kati ya hao walisafirishwa kwenda Hospitali ya Mkoa wa Iringa kwa matibabu zaidi.
Genge la uhalifu ‘yahoo boys’ mikononi mwa polisi
“Tumepokea miili ya hao marehemu na majeruhi nane lakini majeruhi wawili tumewahamishia Hospitali ya Mkoa wa Iringa kwa ajili ya matibabu zaidi,” alithibitisha Daktari Msafiri.
Aidha, kupitia taarifa iliyotolewa kwa Wanahabari, Rais Samia amevitaka vyombo vinavyosimamia usalama wa Barabarani, kuendelea kutoa elimu kwa madereva ili wazingatie sheria.
Mwaka 2015 katika eneo hilo, ilitokea ajali nyingine ya basi la Majinja lililoangukiwa na kontena la lori na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 40 na wengine 23 kujeruhiwa.