Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amepiga kura yake katika kituo cha Mutomo kilichopo Gatundu Kusini, akiameambatana na mkewe, Margaret Kenyatta.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kupiga kura Rais alieleza kuwa shughuli hiyo ilikuwa shwari, akiwataka Wakenya kujitokeza kwa wingi na kupiga kura.
Pia ameongeza kuwa Wakenya wanapaswa kuipa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) muda na nafasi ya kujumlisha na kutangaza matokeo.
Uhuru, ametoa wito kwa Wakenya kuweka utulivu wakati wote wa uchaguzi akibainisha kuwa shughuli hiyo itakuwa huru na haki.
“Mchakato ulikuwa mwepesi, mchakato haukuchukua muda mrefu, kila kitu kinaonekana kufanya kazi tunatumai itaendelea hivyo kwa siku nzima,” amesema Uhuru Kenyatta.
“Pigeni kura na piga kura kwa amani na kila Mkenya na mimi binafsi tunaamini kuwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki.”
Rais Kenyatta, anatarajiwa kuachia madaraka baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa mihula miwili.
Hapo awali, mama yake na Rais Kenyatta Mama Ngina Kenyatta, alifika katika uwanja huo ili kupiga kura.