Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kufuatia ajali ya barabara iliyosababisha vifo vya watu 11 na wengine 15 kujeruhiwa.
“Nimepokea kwa mshtuko taarifa ya vifo vya watu 11 vilivyotokea leo jioni (Septemba 7, 2018) huko Mbeya, kwa mara nyingine tumewapoteza Watanzania wenzetu katika ajali ya barabarani na wengine wameumia, nimesitishwa sana na vifo hivi.” amesema Rais Magufuli.
Kwa masikitiko Rais Magufuli amewapo pole wanafamilia waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo. “Nawapa pole wanafamilia wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hii na pia nawapa pole majeruhi wote, nawaombea watibiwe na kupona haraka ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku” Rais Magufuli
Ajali hiyo imetokea Septemba 7, 2018 katika mteremko wa mlima wa Igawilo Jijini Mbeya baada ya Lori lililokuwa na shehena ya viazi, likitokea Tukuyu kwenda Mbeya Mjini kuyagonga magari matano likiwemo basi dogo lililokuwa na abiria.
Rais Magufuli amewaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi.
Dar24 Media pia tunatoa pole kwa wote walioguswa pamoja na watanzania wote. Wapumzike kwa amani. Amen