Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameeleza jinsi alivyopokea kwa mshtuko taarifa za kifo cha muasisi wa Taifa la Zimbabwe, Robert Mugabe.
Akitoa salamu zake za rambirambi, Rais Magufuli amesema Afrika imepoteza mmoja kati ya viongozi jasiri, shupavu na aliyekataa ukoloni kwa vitendo.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe Mzee Robert Mugabe. Afrika imepoteza mmoja wa viongozi Jasiri, Shupavu, Mwanamajumui wa Afrika na aliyekataa ukoloni kwa vitendo. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina,” ameandika Rais Magufuli.
Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe Mzee Robert Mugabe. Afrika imepoteza mmoja wa viongozi Jasiri, Shupavu, Mwanamajumui wa Afrika na aliyekataa ukoloni kwa vitendo. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.
— Dr John Magufuli (@MagufuliJP) September 6, 2019
Mugabe aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zimbabwe amefariki leo, Septemba 6, 2019 akiwa nchini Singapore alipokuwa akipatiwa matibabu kutokana na maradhi ambayo hayakuwekwa wazi. Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa alisema kuwa Mzee Mugabe anasumbuliwa na maradhi yanayotokana na uzee.
Mwanamageuzi huyo aliyekuwa Rais wa Zimbabwe tangu mwaka 1980 hadi 2017 alipolazimika kujiuzulu, amefariki akiwa na umri wa miaka 95.
Akitangaza kifo cha Mugabe, Rais Mnangagwa alieleza kuwa wamepoteza muasisi aliyekuwa alama ya ukombozi ya taifa hilo.
“Kwa majonzi makubwa, natangaza kifo cha Muasisi na Baba wa Taifa la Zimbabwe, Robert Mugabe. Mugabe alikuwa alama ya ukombozi. Mpigania uhuru wa Afrika aliyejitolea maisha yake kwa ajili ya kuwainua watu. Mchango wake kwa Taifa hili na Bara hili hautasahaulika. Roho yake na ipumzike kwa amani,” aliandika kupitia akaunti yake ya Twitter.
-
Robert Mugabe afariki dunia, Rais wa Zimbabwe amlilia
-
Waziri Mkuu wa Sudan atangaza baraza la Mawaziri