Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameiagiza Wizara ya Kilimo pamoja na Mamlaka zingine zinazohusika kushughulikia hati ya eneo la ardhi lililopo Kata ya Kwembe lenye ukubwa wa ekari 52 ndani ya wiki hii na kuikabidhi kwa Mbunge na uongozi wa jimbo la Kibamba jijini Dar es Salaam.
Rais magufuli ametoa agizo hilo leo Februari 24, 2021 wakati akizindua Kituo kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani na nchi jirani cha Magufuli ambacho kabla ya kuzinduliwa kilijulikana kama kituo cha Mabasi cha Mbezi Luis (jina la sehemu kilipo kituo).
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Issa Mtemvu alimuomba Rais magufuli aweze kuwapatia eneo hilo ili waweze kujenga Uwanja mkubwa wa michezo (sports arena) ambao pia utatumika kwa Mikutano mikubwa ya hadhara pamoja na kusogeza karibu huduma nyingine za kijamii.
Aidha, akizungumza baada ya uzinduzi huo Rais Magufuli ametaka Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Seleman Jafo ambaye ndiye ameamua kuipa stendi hiyo jina la Rais magufuli kuhakikisha kituo hicho kinawapa haki sawa watu wote bila kuwabagua ikiwa ni pamoja na wasafiri pamoja na wafanyabiashara.
“Nimeshangaa Jafo kuandika Stand hii ya Mbezi Luis kwa jina langu maana angeweza kuandika Jafo Stand, sifurahii sana majina yangu kutumika kwa sababu naogopa kitu kimoja, mnaweza kuandika jina langu halafu wananchi masikini, wamachinga wakawa wananyanyaswa hapa,” amesema Rais Magufuli.
“Mimi nilichaguliwa na wananchi hawa wanyonge lakini mara nyingi vitu hivi vizuri vikikamilika wamachinga wanafukuzwa, watu wa kawaida wanafukuzwa, nitaumia sana kama wananchi hawa wanyonge watakuwa wanafukuzwa halafu mmeandika stendi ya Magufuli,” amesema rais Magufuli.
“Mkiwafukuza wamachinga hapa wakati Stand imeandikwa Stand ya Magufuli itaonesha Magufuli ndiye anawafukuza, sitokubali, nikueleze Waziri Jafo inawezekana umejichongea kwa kuiita stendi hii Magufuli, nataka yafanyike ambayo mimi Magufuli nataka,” amesisitiza Rais Magufuli.
Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli ambacho kilianza kujengwa Januari 11, 2019 kimegharimu Shilingi za Kitanzania Bilioni 50.9 mpaka kukamilika kwake na kina uwezo wa kupakia mabasi 108 kwa wakati mmoja na kupokea mabasi 3456 kwa siku.