Wakati Kikosi cha Primeiro De Agosto kikitarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam leo Ijumaa (Oktoba 14) kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Simba SC, Uongozi wa klabu hiyo ya Angola umewaahidi ‘DONGE NONO’ Wachezaji wao endapo watapindua meza na kutinga Hatua ya Makundi.
Primeiro De Agosto itacheza mchezo wa Mkondo wa Pili Jumapili (Oktoba 16) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza nyumbani kwa mabao 3-1 mwishoni mwa juma lililopita (Jumapili-Oktoba 09).
Taarifa kutoka Luanda-Angola zinaeleza kuwa, Rais wa klabu hiyo ?, Gen Carlos ametoa ahadi kwa Wachezaji walioanza safari ya kuja Tanzania ya Dola za Marekani ‘USD $’ 5,000 kwa kila mmoja, endapo wataifunga Simba SC na kutinga Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Fedha hizo ni sawa na Shilingi za Tanzania Milioni 12, ambazo zimeahidiwa kama Motisha kwa Wachezaji, ambao watatakiwa kushinda 2-0 ama zaidi ili kuitoa Simba SC, itakayokua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao hutumika kama Ngome ya Ushindi kwa miamba ya Msimbazi.
Katika mchezo wa Jumapili (Oktoba 16), Simba SC itatakiwa kulinda ushindi wake wa 3-1, kwa kusaka sare ama ushindi wa aina yoyote, ili itinge Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Hata hivyo Primeiro De Agosto imekua na Rekodi nzuri inapocheza ugenini, kwani mchezo uliopita dhidi ya Red Arrows ya Zambia iliambulia ushindi wa 2-1, kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani kwao Luanda-Angola.