Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele amewatuliza Mashabiki wa Klabu ya Young Africans kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Young Africans iliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Al Hilal mwishoni mwa juma lililopita (Jumapili-Oktoba 08), hali ambayo ilizua taharuki kwa Mashabiki wa klabu hiyo, wakiamini timu yao haitaweza kufurukuta ugenini mjini Khatoum.

Mayele amesema, bado safari ya kwenda makundi haijamalizika kwani wanao uwezo wa kusonga mbele wakiwa ugenini huku akiwataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwapa moyo wa kupambana.

“Mashabiki tunajua jinsi gani walivyoumizwa na matokeo ya sare tukiwa nyumbani, na kwa kiasi kikubwa tunafahamu kuwa haikuwa matarajio yetu kupata sare.”

“Tunawahakikishia mashabiki wetu kuwa tutapambana katika mchezo ujao ambao tutakuwa ugenini kuhakikisha kuwa tunaibuka na matokeo, tunawaomba mashabiki wasitukatie tamaa,” amesema Mayele

Young Africans inatarajia kuondoka Dar es salaam kesho Jumamosi (Oktoba 15) kuelekea Khatoum-Sudan kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Jumapili (Oktoba 16) katika Uwanja wa Al Hilal.

Young Africans inatakiwa kupata ushindi wa aina yoyote ama sare ya 2-2 na kuendelea ili kutinga hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.

Taifa lisilo na utamaduni wake ni Taifa mfu: Julius K. Nyerere
Young Africans yawajibu wachambuzi, kusafiri kesho