Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema mradi wa ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi rasi ya Chongoleani Tanzania (EACOP) utachochea uwekezaji, biashara na kufungua milango ya fursa katika nchi za Uganda na Tanzania.
Rais Samia amesema hayo leo wakati wa hotuba yake mbele ya wadau wa mradi huo wakati wafla ya kusainiwa mkataba wa utatu, unaohusisha kuanza upande wa Serikali na Kampuni ili kuanza ujenzi wa bomba hilo la kilometa 1,445.
Bomba hilo lenye sehemu ya asilimia 80 upande wa Tanzania, litajengwa na kuendeshwa na Kampuni ya Bomba la Mafuta ikiwa ni ubia wa Kampuni ya Mafuta ya Uganda (UNOC), Shirika la Maendeleo la Petroli la Tanzania(TPDC) na Kampuni mbili za mafuta, Total na CNOOC.
“Mradi huu utakuwa na manufaa ya kiuchumi na kijamii, kwa pande zote mbili(Uganda na Tanzania), utaongeza mapato kwa serikali zetu, na utatengeneza ajira za muda mfupi na mrefu, inakadiriwa zaidi ya ajira 10,000 zitapatikana,” amesema Rais Samia.
Kabla ya kueleza manufaa hayo, Rais Samia alieleza mchango wa Hayati Rais John Magufuli katika hatua za upatikanaji wa mradi kutoka serikali ya Uganda na ufanikishaji wa mazungumzo kabla ya kuanza mradi huo utakaogharimu thamani ya Dola bilioni 3.5 za Marekani.
“Makubaliano yanayofanyika leo yalitakiwa kufanyika mwezi uliopita lakini baada ya kifo cha Rais wetu John Magufuli ulisitisha (akimweleza rais Yower Museveni), hatua hiyo ilionyesha urafiki wa kweli, tunashukuru sana,” amesema Rais Samia.