Rais Samia Suluhu Hassan, ameipongeza timu ya Yanga kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika (CAF) huku akibainisha kuwa kitendo hicho kimeitoa nchi kimasomaso na kuipandisha hadhi Tanzania katika viwango vya soka.
Akizungumza jana Jumatatu (Juni 05) Ikulu, Dar es Salaam, wakati wa hafla aliyoiandaa kuipongeza timu hiyo kwa hatua iliyofikia, Rais aliahidi kuwa serikali itakuwa pamoja na wanamichezo wote wakati wowote kwa ajili ya kuwaunga mkono na kuwapa msaada wa hali na mali pale watakapokuwa wakiiwakilisha nchi.
“Ndugu zangu mmefika fainali, lakini kama walivyosema ni mambo ya kikanuni, vinginevyo tungekuwa tunaongea mengine hapa.
“Kwa kweli mmetutoa kimasomaso na mnastahili pongezi sana. Hongereni sana. Natambua matokeo haya hayakuja kwa kubahatisha, bali ni jitihada za wachezaji, walimu, kocha Nabi (Nasreddine) na timu yake, benchi la ufundi pia wadhamini wa timu, Kamati ya Utendaji, Wizara na Watanzania wote kwa ujumla,” alisema.
Aliipongeza Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano ilioutoa kwa klabu zote mbili za Simba na Yanga wakati zikicheza michuano ya kimataifa mpaka moja (Simba) ilipotolewa Ligi ya Mabingwa na Yanga kubaki kwenye Kombe la Shirikisho hadi mwisho wa safari.
“Kufika fainali kwa Yanga kwenye mashindano haya kumeiletea nchi yetu heshima na kuturudisha kwenye ramani ya kisoka. Mara kadhaa nilikuwa nasema nataka kuirudisha.
Tanzania kwenye heshima yake pale inapotakiwa kukaa. Sasa kwa upande wa michezo tumefanya kazi kubwa na nzuri na nchi imerudi tena kwenye ramani yake ya michezo. Iwe kwenye soka, riadha, tunakwenda na tutafika inapopaswa kukaa.
“Haikuwa kazi rahisi kwa sababu na nchi nyingine zilishiriki lakini mwisho ya siku ni timu kutoka Tanzania ndiyo iliyofika ikicheza na Waalgeria… Klabu hii sasa imeandika historia ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika na kama nilivyosema si jambo dogo wala jepesi.
“Niwaombe sasa viongozi wote, mwendelee kuwapa ari na motisha vijana wetu hasa kwa kuangalia maslahi yao. Kama yakitekelezwa timu zetu huwa zinafanya vizuri kwa sababu historia inaonyesha kuwa mwaka 1993, Simba nayo ilifika kwenye kiwango hiki (fainali za Kombe la CAF, maarufu kama Kombe la Abiola),” alisema Rais.
Katika hatua nyingine, Rais Samia aliendelea kusisitiza azma ya Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ikishirikiana na nchi za Kenya na Uganda.
Kutokana na azma hiyo, aliielekeza wizara husika kuendelea na ujenzi ya viwanja vipya na kurekebisha vilivyopo, ukiwamo wa Amaan, Zanzibar.
Wakati huo huo, aliiwaagiza viongozi wa Yanga kumaliza sintofahamu ya kimkataba iliyopo kati ya klabu hiyo na mchezaji, Feisal Salum.
“Nina ombi kwenu, sifurahii kusikia mnakuwa na mizozo na wachezaji, sitaki kusema mengi, nataka niwaambie tu kuwa hii inshu ya Fei Toto (Feisal) kaimalizeni. Kamalizeni ili tuangalie mbele sasa. Haipendezi klabu nzuri kama hii iliyofanya kazi nzuri mnakuwa na kaugomvi na katoto. Nitasubiri kupata mrejesho wa hili,” alisema.