Rais wa Jamhuti ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema asilimia 90 ya ajali za barabarani zinazotokea nchini Tanzania husababishwa na makosa ya kibinadamu ambayo yanaweza kuzuilika, na kuwataka Jeshi la Polisi kuongeza utoaji wa elimu ili kupunguza athari ambazo Taifa linapata kila mwaka kutokana na ajali hizo.
Akitolea mfano ajali za bodaboda amesema kwa mwaka watu 400 hufariki nchini, huku 800 wakipata madhara mbalimbai kutokana na ajali hizo.
Aidha Rais Samia ametoa maagizo matano kwa Jeshi la Polisi ikiwemo suala la kuongeza utoaji elimu ya usalama barabarani kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu ili kila mtumiaji wa barabara azifahamu taratibu, lakini pia kutumia zaidi mitandao ya kijamii kwani vijana ambao ni walengwa wakubwa wakati mwingine hawatazami televisheni wala kusikiliza redio.
Ameagiza utafiti kufanyika ili kuwezesha kupatikana kwa suluhu ya kisayansi ya kupunguza ajali barabarani, ameelekeza hilo kufanyika kwa kushirikiana na vyuo mbalimbali nchini huku akiwatak askari polisi wawe chanzo cha usalama barabarani kwa kuhakikisha kunapokuwa na tatizo, wananchi wanawakimbilia na sio kuwakimbia.
Pia ameelekeza polisi kutokushikilia leseni za madereva kinyume na sheria, huku akiagiza polisi kutokuwalazimisha madereva kulipa faini papo hapo wanapokamatwa. Ameeleza kushangazwa na vyombo vingi vya usafiri, mathali pikipiki ambazo zimejazana kwenye vituo vya polisi, na hivyo kutaka lifanyiwe kazi, kesi au faini ikilipwa ziachiwe.
Katika agizo la tano Rais Samia amewataka wananchi kuchukua wajibu wa kuzuia ajali kwa kuzingatia sheria za barabarani wanapotumia vyombo vya moto na kutoa taarifa pindi mtumiaji mwingine anapovunja sheria.