Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAmia Suluhu Hassan amewaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kuhakikisha wanawasimamia vizuri Wafanyabiashara wadogo maarufu kama (Wamachinga) ikiwa ni pamoja na kuwatengea maeneo ambayo hayatakuwa na bughudha kwao na kwa wengine.
Ametoa agizo hilo leo Septemba 13, 2021 Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, wakati wa hafla ya kuwaapisha Mawaziri wanne pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha amewaagiza wakuu hao kuandaa mipango mizuri itakayowawezesha Wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao kwa mpangilio na si kama hali ilivyo sasa.
Hata hivyo Rais Samia ametaka jambo hilo lifanyike bila ya kutumia nguvu na bila ya kumuonea mtu, huku akiwasisistiza wafanyabiashara hao wadogo kufuata sheria zilizopo wakati wanapofanya shughuli zao.
Rais Samia amesema amelazimika kutoa kauli hiyo baada ya kuona katika maeneo mengi Wafanyabiashara hao wamekuwa wakifanya kazi hata katika maeneo yasiyostahili na kuleta usumbufu kwa watu wengine, hali ambayo pia imekuwa ikiikosesha Serikali mapato.