Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa ataunda kamati ya wataalam kuangalia kitaalamu suala la ugonjwa wa Corona ili waweze kuishauri Serikali, huku akisisitiza kuwa taifa halipaswi kuwa kimya, na ni vyema wakalikataa ama kulikubali baada ya kufanya tafiti za kitaalam.
Rais Samia ametoa msimamo huo leo Ikulu Dar es Salaam wakati wa hafla ya uapisho wa Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi za serikali walioteuliwa hivi karibuni.
“Tutaunda Kamati ya Wataalamu kuhusu Covid 19 watuambie kitaalamu hayo yanayopendekezwa na Ulimwengu kuja kwetu yapoje, hatuwezi kujitenga tu kama Kisiwa na hatuwezi kupokea yanayoletwa bila kuweka cha kwetu, bila kufanya utafiti wa kwetu,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameiagiza Wizara ya Afyakupitia wataalam wake kulimaliza suala la bima ya afya kwa wote na kulipeleka serikalini ili liweze kufanyiwa kazi na kumalizika kwa haraka.
“Wataalam wamalize hili watuletee serikalini tulimalize kwa pamoja. Watanzania wanakata bima za afya wakifika hospitalini dawa hakuna, nendeni mkalitazame hili,” amesema Rais Samia.
Kuhusu upungufu wa dawa MSD, Samia ameitaka TAMISEMI kulishughulikia mara moja kwani kumekuwa na upoteaji wa dawa kabla hazijafika hospitalini.
“Huenda TAMISEMI mna madeni, au dawa zinapotelea katikati…. Waganga Wafawidhi, wa Wilaya na Mikoa kuna dawa zinapotea hapo katikati chukueni hatua msioneane aibu,” amesisitiza Rais Samia.