Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Tuzo ya Heshima kutoka kwa waandaji wa tuzo za filamu Tanzania 2022 kutokana na mchango wake katika kukuza Sekta ya Filamu na kuanzisha mfuko wa Utamaduni na Sanaa nchini.
Mara baada ya kutolewa kwa Tuzo hiyo usiku wa Desemba 17, 2022 Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa alitumia nafasi hiyo kutoa siku tano kwa Watendaji kukamilisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa na kuiagiza Idara ya Sanaa na Bodi ya Filamu kuhakikisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa unaanza kutoa mikopo kwa Wasanii ifikapo jumatano ya Desemba 21, 2022.
Amesema, “Sekta ya Filamu inakua, na inaendelea kutoa ajira Kwa vijana wengi pamoja na kuchangia katika Pato la Taifa, hivyo sisi kama Serikali tutaendelea kuweka nguvu katika Sekta hiyo.”
Aidha, Mchengerwa pia amesisitiza Watendaji wa Wizara kumaliza michakato iliyopo katika utekelezaji wa majukumu kwa wadau wa Sekta za Wizara yake, huku akiwaasa kuweka mazingira rahisi kwa wadau hao, kutekeleza majukumu yao.
Tuzo hiyo, ilipokelewa kwa niaba ya Rais Samia na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa ambaye pia alioa Tuzo malaam kwa Wasanii waliofanya vizuri na kutoa mchango wa kukuza kwa Sekta ya Filamu Nchini.