Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika tukio la ufungaji wa lango la handaki mchepuko (diversion tunnel), ili kuruhusu maji yaanze kujaa katika bwawa la kufua umeme la Mwl. Julius K. Nyerere.

Akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo Desemba 18 2022 Waziri wa Nishati, January Makamba amesema mpaka kufikia mwezi Novemba 2022 mradi ulikuwa umefikia asilimia 78.68 na kwamba tukio hilo la ufungaji wa lango linatarajia kufanyika siku ya Alhamisi Desemba 22, 2022.

Waziri wa Nishati, January Makamba, wa pili kushoto akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari.

Amesema, “Mradi huu una hatua kubwa mbili ambazo zina hadhi ya kushuhudiwa na kusherehekewa. Moja ni kufunga lango la njia ya mchepusho wa maji na ya pili ni kuwasha mitambo ya kufua umeme na tunategemea itachukua misimu miwili ya mvua kulijaza bwawa na kuanza kujaribu mitambo.”

Bwawa la Mwalimu Nyerere, litahifadhi lita 33.2 bilioni za maji ambazo zikitumika kwa mitambo yote, itaweza kuendesha mitambo kwa kipindi cha mwaka mmoja na faida ya mradi huo ni kilimo chini ya mto Rufiji, kuondoa mafuriko na kupata umeme wa uhakika.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Desemba 19, 2022
Rais Samia atunukiwa Tuzo ukuzaji sekta ya Filamu