Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo Agosti 28,2021 amezindua miradi mbalimbali ya maendeleo Kizimkazi, Zanzibar katika kilele cha Tamasha la Kizimkazi.
Aidha Rais Samia amezindua ukarabati wa madarasa ya chekechea na ofisi za walimu, Nyumba za madaktari na jengo la ofisi ya maendeleo, pia amepokea gari la kubebea wagonjwa katika Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja .
Pamoja na uzinduzi huo Rais Samia ameongozana na raia wa kigeni kutoka nchi mbalimbali duniani wakiwa na lengo la kutembelea maeneo yenye vivutio vya kitalii visiwani Zanzibar na kwenda kutangaza katika nchi zao.
Hata hivyo Rais Samia amewasisitiza wananchi wa Zanzibar kuendelea kujikinga na maradhi ya COVID 19 na kuwakumbusha kushiriki katika sensa ya watu na makazi ambayo inatarajiwa kufanyika mwakani 2022.
Tamasha la Kizimkazi lina lengo la kuendeleza tamaduni za Wanzanzibari, kuhamasisha shughuli za maendeleo, na Kutangaza fursa za kiuchumi kama kilimo, utalii, na uvuvi.
Leo Agosti 28, 2021 imekua kilele cha Tamasha la Kizimkazi ambalo limedumu kwa wiki moja kwa kushirikisha mafunzo ya wajasiriamali, utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, sanaa, tamaduni na michezo ikiwa ni pamoja kuendelea kutoa chanjo ya COVID 19.