Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amewahimiza Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) kwenye maeneo mbalimbali duniani kuwa na utaratibu wa kujitambulisha na kujiandikisha kwenye Balozi za Tanzania zilizo karibu yao ili kuiwezesha Serikali kuwa na taarifa zao na kuwashirikisha kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi.

Waziri Mulamula ametoa rai hiyo alipokutana kwa mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Kenya katika mkutano uliofanyika kwenye Makazi ya Balozi jijini Nairobi hivi karibuni.

Balozi Mulamula ambaye amefuatana na Mawaziri kadhaa kwenye mkutano huo, amesema kwa sasa Wizara ya Mambo ya Nje ina mpango mahsusi wa kuwatambua Diaspora wote kwa kukusanya taarifa zao na kuzihifadhi katika Kanzidata (Database) kwa lengo la kuiwezesha Serikali kuwa na taarifa muhimu za Watanzania hao hususan elimu, kazi, ujuzi na mitaji ili iwe rahisi kuwashirikisha kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ya taifa.

Aidha Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wa Diaspora kwenye maendeleo ya Taifa na imejipanga kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuwawezesha kuchangia kikamilifu maendeleo ya nchi.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mchango wa Diaspora kwenye maendeleo ya Taifa. Na haya si maneno yangu kwani tayari yameainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 184, sura ya 7 kipengele D pamoja na Sera mpya ya Mambo ya Nje ambayo imejumuisha masuala ya Diaspora,” Amesema Balozi Mulamula.

Hata hivyo Balozi Mulamula ametumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania Kote ulimwenguni kuheshimu sheria za nchi walizopo na kupeperusha bendera ya Tanzania ya maadili mema ambayo inajulikana duniani kote.

“Wapo Watanzania wachache wamefungwa magerezani kwenye nchi mbalimbali kwa makosa ya uvunjifu wa sheria. Tafadhali nawaomba mfuate sheria kwenye nchi mlizopo na mbebe bendera ya Tanzania ya tabia njema ambayo inajulikana duaniani” Amesema Balozi Mulamula.

Katika hatua nyingine Waziri Mulamula ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha Diaspora hao kuchangamkia fursa ya kuanzisha vituo vya Kiswahili kwenye nchi walizopo ili kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa inayouzika, lakini pia kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutangaza biashara, uwekezaji, utalii na bidhaa za Tanzania ili kuchangia maendeleo ya nchi.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambaye amefuatana na Waziri Mulamula nchini Kenya amewahimiza Diaspora wanaohitaji ardhi kuja nchini na kufika Wizarani kwake ili kupata ufafanuzi wa kina wa masuala ya ardhi badala ya kutafuta taarifa nje ya utaratibu na kujikuta wanatapeliwa fedha zao.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania waishio Kenya, Padri Cleophas Tesha amemshukuru Balozi Mulamula, kwa kutenga muda wa kuzungumza na Jumuiya hiyo na kumwomba kuendelea kuwashirikisha Diaspora kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Diaspora hao.

Rais Samia afungua kikao kazi cha tathmini ya mwaka mmoja jeshil la polisi
Uzi mpya Young Africans 2021/22